Kiswahili

Yeye Hana Budi Kukua; Mimi Sina Budi Kupungua

11 Januari 2020
Jumamosi baada ya Epifania
Masomo ya Leo

Sikiliza kwa Kiingereza

“Yeye hana budi kukua; mimi sina budi kupungua.”  Yohane 3:30

Maneno haya yenye nguvu na ya kinabii ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji yanapaswa kusikika mioyoni mwetu kila siku.  Yanatusaidia kuweka mwelekeo wa maisha yetu yote na wa namna tunavyopaswa kuwa.  Maneno haya yanamaanisha nini?  Ni wazi kwamba Yohane anasema mambo mawili hapa: 1) Yesu hana budi kukua, 2) Sisi hatuna budi kupungua.

Kwanza kabisa, kukua kwa Yesu katika maisha yetu ndilo lengo kuu tunalopaswa kuwa nalo.  Hili hasa linamaanisha nini?  Linamaanisha kwamba anatawala zaidi akili na utashi wetu.  Linamaanisha kwamba sisi ni Wake na Yeye ni wetu.  Linamaanisha kwamba lengo na hamu yetu kuu maishani ni kutimiza mapenzi Yake matakatifu katika mambo yote.  Linamaanisha kwamba hofu inaondolewa na mapendo yanakuwa sababu yetu ya kuishi.  Kumruhusu Bwana akue katika maisha yetu kunatuletea uhuru mkubwa.  Kunatuletea uhuru kwa maana kwamba hatuhitaji tena kujaribu kuendesha maisha kwa nguvu zetu wenyewe.  Sasa Yesu anaishi ndani yetu na kwa njia yetu.

Pili, Yohane anaposema kwamba hana budi kupungua, anamaanisha kwamba utashi wake mwenyewe, matamanio yake, matarajio yake makubwa, matumaini yake, na kadhalika, havina budi kuyeyuka kadiri Yesu anavyochukua usukani.  Inamaanisha kwamba ubinafsi wote hauna budi kuachwa, na kuishi bila ubinafsi hakuna budi kuwa kanuni ya msingi ya maisha yetu.  “Kupungua” mbele ya Mungu kunamaanisha kuwa wanyenyekevu.  Unyenyekevu ni njia ya kuacha kila kitu kisichotoka kwa Mungu na kumruhusu Mungu pekee aangaze kupitia sisi.

Tafakari leo kauli hii nzuri ya Mtakatifu Yohane Mbatizaji.  Ifanye kuwa sala na uirudie tena na tena.  Iache iwe kanuni inayoongoza maisha yako.

Bwana, Wewe huna budi kukua nami sina budi kupungua.  Tafadhali njoo uitawale roho yangu kikamilifu.  Badilisha akili na moyo wangu, uongoze utashi wangu, hisia zangu na matamanio yangu.  Na unijalie kuwa chombo kitakatifu cha uzima Wako wa kimungu.  Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu za Leo