Januari 19, 2020
Jumapili ya Pili ya Kipindi cha Kawaida, Mwaka A
Masomo ya Leo

Sikiliza kwa Kiingereza
Yohane Mbatizaji alimwona Yesu akimjia, akasema, “Tazama, Mwanakondoo wa Mungu, anayeondoa dhambi ya ulimwengu. Huyu ndiye niliyesema habari zake, ‘Nyuma yangu anakuja mtu aliye mkuu kuliko mimi, kwa sababu alikuwako kabla yangu.’” Yohane 1:29-30
Ajabu kweli! Utambuzi aliokuwa nao Mtakatifu Yohane Mbatizaji kuhusu Yesu unatia moyo sana, una fumbo na unastaajabisha. Anamwona Yesu akimjia na mara moja anataja kweli tatu zilizofunuliwa kuhusu Yesu: 1) Yesu ni Mwanakondoo wa Mungu; 2) Yesu ni mkuu kuliko Yohane; 3) Yesu alikuwako kabla ya Yohane.
Yohane angewezaje kujua haya yote? Kauli hizi zenye kina kuhusu Yesu zilitokana na nini? Inawezekana sana kwamba Yohane alikuwa amejifunza Maandiko yaliyokuwapo wakati huo na alijua kauli nyingi kuhusu Masihi ajaye zilizotamkwa na manabii wa kale. Angekuwa anazijua Zaburi na Vitabu vya Hekima. Lakini, kwanza kabisa, Yohane angekuwa ameyajua hayo kwa kipawa cha imani. Angekuwa amepewa na Mungu utambuzi wa kweli wa kiroho.
Ukweli huu hauonyeshi tu ukuu wa Yohane na kina cha imani yake, bali pia unaonyesha mfano bora tunaopaswa kujitahidi kuufuata maishani. Tunapaswa kujitahidi kila siku kuenenda kwa utambuzi halisi wa kiroho tunaofadhiliwa na Mungu.
Si kwamba ni lazima tuishi, siku baada ya siku, katika hali fulani iliyo dhahiri, ya kinabii na ya kifumbo. Si kwamba tunapaswa kutarajia kuwa na maarifa yaliyo juu kuliko ya wengine. Bali tunapaswa kuwa tayari kupokea Vipawa vya Roho Mtakatifu ili tupate maarifa na ufahamu wa maisha unaozidi yale ambayo akili ya mwanadamu peke yake inaweza kupata kwa juhudi zake yenyewe.
Ni wazi kwamba Yohane alijawa na Hekima, Ufahamu, Shauri, Elimu, Nguvu, Uchaji na Kustaajabu. Vipawa hivi vya Roho vilimpa uwezo wa kuishi maisha yaliyotegemezwa na neema ya Mungu. Yohane alijua na kuelewa mambo ambayo Mungu pekee angeweza kuyafunua. Alimpenda na kumheshimu Yesu kwa ari na kwa kusalimisha utashi wake, mambo ambayo Mungu pekee angeweza kumvuvia. Ni dhahiri kabisa kwamba utakatifu wa Yohane ulitokana na muungano wake na Mungu.
Tafakari leo kauli hii ya Yohane kuhusu Yesu, yenye utambuzi wa pekee sana. Yohane alijua aliyoyajua kwa sababu tu Mungu alikuwa hai katika maisha yake, akimwongoza na kumfunulia kweli hizi. Jitoe leo kuiga imani ya kina ya Yohane, na uwe tayari kupokea yote ambayo Mungu anataka kukuambia.
Bwana wangu Yesu mpendwa, nijalie utambuzi na hekima ili nikujue na kukuamini. Nisaidie, kila siku, kuifahamu kwa ukamilifu zaidi fumbo kuu la Wewe ni nani, fumbo linalojaza moyo kicho. Nakupenda, Bwana wangu, nami ninaomba nizidi kukujua na kukupenda. Yesu, nakutumainia.
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu




