5 Agosti 2020
Jumatano ya Juma la Kumi na Nane la Mwaka
Masomo ya Leo
Kuwekwa Wakfu kwa Basilika la Mtakatifu Maria Mkuu—Kumbukumbu ya Hiari

Sikiliza kwa Kiingereza
Lakini yule mwanamke alikuja akamsujudia, akisema, “Bwana, nisaidie.” Naye akajibu, “Si vema kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” Mwanamke akasema, “Tafadhali, Bwana, maana hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka mezani pa mabwana wao.” Mathayo 15:25-27
Je, kweli Yesu alimaanisha kwamba kumsaidia mwanamke huyu kulikuwa kama kuwatupia mbwa chakula? Wengi wetu tungeudhika sana kwa maneno ya Yesu kwa sababu ya kiburi chetu. Lakini aliyosema yalikuwa kweli, wala hayakuwa ya kifidhuli kwa namna yoyote. Ni wazi kwamba Yesu hawezi kuwa mfidhuli. Hata hivyo, kwa juu juu, kauli Yake inaonekana kuwa ya kifidhuli.
Kwanza, tuangalie jinsi kauli Yake ilivyo ya kweli. Mwanamke huyu alikuwa akimwomba Yesu aje kumponya binti yake. Kimsingi, Yesu anamwambia kwamba hastahili neema hii kwa namna yoyote. Na huo ndio ukweli. Kama vile mbwa asivyostahili kulishwa kutoka mezani, sisi pia hatustahili neema ya Mungu. Ingawa hii ni namna ya kushtua ya kueleza jambo hilo, Yesu anasema hivyo ili kwanza kuonyesha ukweli wa hali yetu ya dhambi na kutostahili kwetu. Na mwanamke huyu anakubali hilo.
Pili, kauli ya Yesu inampa mwanamke huyu nafasi ya kuitikia kwa unyenyekevu na imani kubwa kabisa. Unyenyekevu wake unaonekana katika kutokataa kwake kufananishwa na mbwa anayekula kutoka mezani. Badala yake, anaeleza kwa unyenyekevu kwamba hata mbwa hula makombo. Ama kweli, huu ni unyenyekevu! Kwa hakika, tunaweza kuwa na uhakika kwamba Yesu alizungumza naye kwa namna hii iliyomshusha kiasi kwa sababu alijua jinsi alivyokuwa mnyenyekevu, na alijua kwamba angeitikia kwa kuuacha unyenyekevu wake uangaze ili kuidhihirisha imani yake. Hakuudhishwa na ukweli uliomnyenyekeza kuhusu kutostahili kwake; badala yake, aliukubali na pia akatafuta huruma tele ya Mungu licha ya kutostahili kwake.
Unyenyekevu una uwezo wa kuifungua njia kwa imani, nayo imani huifungua njia kwa huruma na nguvu za Mungu kutenda kazi. Mwishowe, Yesu anasema ili wote wasikie, “Ee mwanamke, imani yako ni kubwa!” Imani yake ilidhihirika, naye Yesu akaitumia nafasi hiyo kumheshimu kwa sababu ya imani hiyo yenye unyenyekevu.
Tafakari leo kuhusu unyenyekevu wako mwenyewe mbele za Mungu. Ungeitikiaje kama Yesu angezungumza nawe kwa namna hii? Je, ungekuwa na unyenyekevu wa kutosha kukiri kutostahili kwako? Ikiwa ndivyo, je, ungekuwa pia na imani ya kutosha kuililia huruma ya Mungu licha ya kutostahili kwako? Sifa hizi nzuri sana huenda pamoja (unyenyekevu na imani) na kuifungua njia kwa huruma ya Mungu kutenda kazi!
Bwana, mimi sistahili. Nisaidie kulitambua hilo. Nisaidie kutambua kwamba sistahili neema Yako maishani mwangu. Lakini katika ukweli huo unaoninyenyekeza, nijalie pia kutambua wingi wa huruma Yako na nisiogope kamwe kukuomba huruma. Yesu, nakutumainia.
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Mtakatifu wa Siku – Kuwekwa Wakfu kwa Basilika la Mtakatifu Maria Mkuu
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu
Picha: Yule Mwanamke wa Kanaani Miguuni pa Kristo iliyochorwa na Jean Germain Drouais




