Kiswahili

Kumwalika Yesu

Oktoba 30, 2020
Ijumaa ya Juma la Thelathini la Mwaka
Masomo ya Leo

Sikiliza kwa Kiingereza

Siku ya sabato Yesu alikwenda kula nyumbani kwa mmoja wa viongozi wa Mafarisayo, na watu waliokuwapo walikuwa wakimtazama kwa makini.  Luka 14:1

Sentensi hii, iliyo mwanzoni mwa Injili ya leo, inafunua mambo mawili yanayostahili kutafakariwa.

Kwanza, Yesu alikwenda kula nyumbani kwa mmoja wa viongozi wa Mafarisayo.  Hili halikuwa jambo dogo.  Kwa kweli, inaelekea sana kwamba lilizua mazungumzo mengi miongoni mwa watu na Mafarisayo wengine.  Linatuonyesha kwamba Yesu hana upendeleo.  Hakuja kwa ajili ya maskini na wanyonge tu.  Alikuja pia ili matajiri na wenye mamlaka waongoke.  Mara nyingi mno tunasahau ukweli huo ulio wazi.  Yesu alikuja kwa ajili ya watu wote, anawapenda watu wote na anaitikia mialiko ya wote wanaotaka awepo katika maisha yao.  Bila shaka, kifungu hiki pia kinafunua kwamba Yesu hakuogopa kuja nyumbani kwa kiongozi huyu wa Mafarisayo na kumpa yeye pamoja na wageni wake changamoto ili kuwachochea wabadili mioyo yao.

Pili, kifungu hiki kinasema kwamba watu walikuwa “wakimtazama kwa makini.”  Huenda wengine walikuwa na udadisi tu na walikuwa wakitafuta jambo la kuzungumzia baadaye na rafiki zao.  Lakini inaelekea sana kwamba wengine walikuwa wakimtazama kwa makini kwa sababu walitaka kweli kumwelewa.  Walitambua kwamba kulikuwa na jambo la pekee kuhusu Yesu, nao walitaka kumfahamu zaidi.

Mafundisho haya mawili yanapaswa kututia moyo tutambue kwamba Yesu anatupenda kweli na ataitikia utayari wetu wa kuupokea uwepo Wake katika maisha yetu.  Tunachopaswa kufanya ni kumwomba tu na kuwa tayari kumpokea anapokuja “kula” pamoja nasi.  Tunapaswa pia kujifunza kutokana na ushuhuda wa wale waliokuwa wakimtazama kwa makini.  Wanatuonyesha hamu njema tunayopaswa kuwa nayo ya kuendelea kumkazia Yesu macho yetu.  Ingawa baadhi ya waliomtazama kwa makini walimgeuka na kumdhihaki, kulikuwa na wengine waliomtazama kwa makini na kumpokea Yesu pamoja na ujumbe Wake.

Tafakari leo juu ya utayari wako wa kumwalika Yesu ndani ya nyumba ya moyo wako na katika hali ya maisha yako.  Jua kwamba atakubali mwaliko wowote unaompa.  Na Yesu anapokuja kwako, mwelekee kwa usikivu wako wote.  Angalia yote anayosema na kutenda, na uache uwepo Wake na ujumbe Wake viwe msingi wa maisha yako.

Bwana, ninakualika kwa moyo wote uingie moyoni mwangu.  Ninakualika katika kila hali ya maisha yangu.  Tafadhali njoo ukae nami katika familia yangu.  Njoo ukae nami kazini, miongoni mwa rafiki zangu, katika shida zangu, wakati wa kukata tamaa kwangu, na katika mambo yote.  Nisaidie nikusikilize Wewe na kuyatambua mapenzi Yako, na uniongoze kufikia yote uliyoniandalia katika maisha yangu.  Yesu, nakutumainia.

Sala & Nyenzo kwa ajili ya Uchaguzi wa Marekani

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha: Kristo Nyumbani kwa Simoni Mfarisayo, iliyochorwa na Pierre Hubert Subleyras