Kiswahili

Kushinda Vitisho

Oktoba 29, 2020
Alhamisi ya Juma la Thelathini la Mwaka
Masomo ya Leo

Sikiliza kwa Kiingereza

Baadhi ya Mafarisayo walimjia Yesu na kusema, “Ondoka, toka katika eneo hili kwa sababu Herode anataka kukuua.” Akajibu, “Nendeni mkamwambie yule mbweha, ‘Tazama, ninatoa pepo na kuponya watu leo na kesho, na siku ya tatu ninatimiza kusudi langu.’”  Luka 13:31-32

Mazungumzo haya kati ya Yesu na baadhi ya Mafarisayo yanavutia sana.  Inavutia kutazama matendo ya Mafarisayo na pia yale ya Yesu.

Tunaweza kujiuliza kwa nini Mafarisayo walizungumza na Yesu kwa namna hii, wakimwonya kuhusu nia ya Herode.  Je, walikuwa na wasiwasi juu ya Yesu na kwa hiyo walikuwa wakijaribu kumsaidia?  Pengine sivyo.  Badala yake, tunajua kwamba Mafarisayo wengi walikuwa na wivu na husuda dhidi ya Yesu.  Katika hali hii, inaonekana kwamba walikuwa wakimwonya Yesu kuhusu ghadhabu ya Herode ili kujaribu kumtisha aondoke katika eneo lao.  Bila shaka, Yesu hakutishwa.

Nyakati nyingine tunapatwa na jambo kama hilo.  Wakati mwingine mtu anaweza kuja kutueleza porojo zinazosemwa kutuhusu, akijifanya kuwa anajaribu kutusaidia, ilhali kwa kweli hiyo ni njia ya hila ya kututisha ili kutujaza hofu au wasiwasi.

La msingi ni kuitikia tu kwa namna ile ambayo Yesu aliitikia alipokabiliwa na upumbavu na nia mbaya.  Yesu hakukubali kutishwa.  Hakusumbuliwa hata kidogo na nia mbaya ya Herode.  Badala yake, alijibu kwa namna ambayo, kwa maana fulani, iliwaambia Mafarisayo, “Msipoteze muda wenu kujaribu kunijaza hofu au wasiwasi.  Ninafanya kazi za Baba yangu, na hilo tu ndilo ninalopaswa kulijali.”

Ni nini kinachokusumbua maishani?  Ni nini kinachokutisha?  Je, unaruhusu maoni, nia mbaya au porojo za wengine zikuvunje moyo?  Jambo pekee tunalopaswa kulijali ni kutimiza mapenzi ya Baba wa Mbinguni.  Tunapotimiza mapenzi Yake kwa kujiamini, tutakuwa pia na hekima na ujasiri tunaohitaji ili kukemea kila udanganyifu na vitisho vya kipumbavu maishani mwetu.

Tafakari leo jinsi unavyojitoa kutimiza mapenzi ya Baba katika maisha yako.  Je, unatimiza mapenzi Yake?  Ikiwa ndivyo, je, unaona kwamba baadhi ya watu huja na kujaribu kukuzuia?  Jitahidi kuwa na ujasiri uleule wa Yesu na uendelee kuelekeza juhudi zako katika utume uliopewa na Mungu.

Bwana, kwa kweli ninayatumainia mapenzi Yako ya kimungu.  Ninautumainia mpango ulioniandalia, nami ninakataa kushawishiwa au kutishwa na upumbavu na nia mbaya za wengine.  Nipe ujasiri na hekima ili niendelee kukutazama Wewe katika mambo yote.  Yesu, nakutumainia.

Sala & Nyenzo kwa ajili ya Uchaguzi wa Marekani

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu