Januari 29, 2022
Jumamosi ya Juma la Tatu la Kipindi cha Mwaka
Masomo ya Leo

Sikiliza kwa Kiingereza
Yesu alikuwa kwenye tezi ya mashua, amelala juu ya mto. Wakamwamsha na kumwambia, “Mwalimu, hujali kwamba tunaangamia?” Akaamka, akaukemea upepo, na kuiambia bahari, “Nyamaza! Tulia!” Upepo ukakoma, kukawa na utulivu mkuu. Marko 4:38-39
Na kukawa na utulivu mkuu! Ingawa maneno haya yanahusu kutulizwa kwa bahari, pia yana ujumbe kuhusu misukosuko tunayokabiliana nayo nyakati fulani maishani. Yesu anataka kuleta utulivu mkuu katika maisha yetu.
Ni rahisi sana kuvunjika moyo maishani. Ni rahisi sana kukazia fikira machafuko yanayotuzunguka. Iwe ni neno kali na lenye kuumiza kutoka kwa mtu mwingine, tatizo la kifamilia, machafuko ya kiraia, mahangaiko ya kifedha, na kadhalika, kuna sababu nyingi zinazoweza kumfanya kila mmoja wetu aangukie katika mtego wa hofu, kukata tamaa, sonona na wasiwasi.
Lakini ilikuwa kwa sababu hii kwamba Yesu aliruhusu tukio hili liwatokee wanafunzi Wake. Aliingia mashuani pamoja na wanafunzi Wake na kuwaruhusu wakumbwe na dhoruba kali wakati Yeye amelala, ili kupitia tukio hili aweze kutupatia sisi sote ujumbe ulio wazi na wenye kusadikisha.
Katika simulizi hili, wanafunzi walikazia fikira jambo moja: Walikuwa wanaangamia! Bahari ilikuwa ikiwatupa huku na kule, nao waliogopa maafa yaliyokuwa karibu kuwakumba. Lakini katika hayo yote, Yesu alikuwapo, amelala fofofo, akingoja wamwamshe. Nao walipomwamsha, aliitawala dhoruba na kuleta utulivu kamili.
Ndivyo ilivyo pia katika maisha yetu. Tunatikiswa kwa urahisi sana na misongo na magumu ya maisha ya kila siku. Mara nyingi sana tunajiruhusu kulemewa na matatizo tunayokabiliana nayo. La msingi ni kuelekeza macho yetu kwa Yesu. Mwone hapo, mbele yako, amelala na akikusubiri umwamshe. Yupo daima, anasubiri daima, yu tayari daima.
Kumwamsha Bwana wetu ni rahisi kama kuacha kuitazama bahari yenye dhoruba na kutumainia uwepo Wake wa kimungu. Jambo kuu ni kumtumainia. Kumtumainia kikamilifu na bila kuyumba. Je, unamtumainia?
Tafakari leo juu ya kile kinachokusababishia wasiwasi, hofu au kuchanganyikiwa kila siku. Ni nini kinachoonekana kukurusha huku na kule, kikikusababishia msongo na mahangaiko? Unapouona mzigo huu, mwone pia Yesu akiwa hapo pamoja nawe, akikusubiri umwendee kwa matumaini ili aweze kutawala kila hali ya maisha unayojikuta ndani yake. Anakupenda na kwa hakika atakutunza.
Bwana wangu uliye usingizini, ninakuelekea Wewe katikati ya changamoto za maisha na ninatamani kukuamsha ili uje kunisaidia. Ninajua kwamba Wewe uko karibu daima, ukinisubiri nikutumainie katika mambo yote. Nisaidie kuelekeza macho yangu Kwako na kuwa na imani katika upendo Wako mkamilifu kwangu. Yesu, nakutumainia.
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Mwaka
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu




