Kiswahili

Gharama ya Uanafunzi

Februari 28, 2022
Jumatatu ya Juma la Nane la Kipindi cha Mwaka
Masomo ya Leo

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

Yesu akamtazama, akampenda na kumwambia, “Unapungukiwa na jambo moja. Nenda, ukauze ulivyo navyo, uwape maskini, nawe utakuwa na hazina mbinguni; kisha njoo, unifuate.” Aliposikia maneno hayo, uso wake ukakunjamana, akaenda zake akiwa na huzuni, kwa maana alikuwa na mali nyingi.  Marko 10:21-22

Kuna mambo mawili muhimu ya kuangazia katika kifungu hiki cha Maandiko Matakatifu.  La kwanza ni mwitikio wa Yesu, na la pili ni mwitikio wa yule kijana tajiri.

Kifungu kinasema kwamba Yesu alimtazama na “akampenda.”  Ni muhimu kuyatambua maneno haya kuwa yanatangulia kile ambacho Yesu anamwita huyu kijana akifanye.  Anamwita aache kila alicho nacho, akigawe chote, kisha aje kumfuata Yesu.  Na Yesu alimwalika kufanya hivyo kwa upendo.

Yesu anamwalika huyu kijana apate mengi zaidi kuliko aliyo nayo sasa.  Ndiyo maana Yesu alimtazama kwa upendo kabla ya kumwalika amfuate kikamilifu na bila kujibakiza.  Lakini katika hali hii, kumpenda Yesu kungeleta maumivu.  Kungeleta maumivu kwa maana kwamba kumfuata Yesu kulimtaka atoe kila kitu sadaka kabisa.  Kulihitaji kujitoa kikamilifu na bila kujibakiza.  Kulikuwa kugumu, angalau kwa mtazamo wa kibinadamu na kidunia tu.  Lakini upendo wa Yesu kwa huyu kijana ulikuwa mkamilifu sana kiasi kwamba alikuwa tayari kumwalika avumilie kujitoa sadaka kwa kuacha kila kitu, ili huyo tajiri aweze kupata mengi zaidi.

Nasi tunaalikwa kufanya vivyo hivyo.  La, huenda tusiitwe kumfuata Yesu kwa njia hiyo ya pekee ya kuacha mali zetu zote bila kubakiza chochote.  Lakini tunaitwa kumfuata Yesu kwa kiwango kilekile cha kutumaini na kujikabidhi kwa mapenzi Yake ya kimungu.  Na hilo bila shaka litahitaji kujitoa sadaka.  Kujitoa sadaka kwa kiwango cha juu kabisa.

Mwitikio wetu kwa wito wa Yesu wa kuwa wanafunzi Wake ni wa msingi.  Tutauitikiaje mwaliko huu wa kujitoa kikamilifu?  Mwitikio wa kwanza wa yule kijana tajiri ulikuwa huzuni.  Hakukubali mwaliko aliopewa na Yesu.  Hatujui kama hatimaye alimfuata Yesu kwa namna hii ya kujitoa kikamilifu na bila kujibakiza, lakini tunajua mwitikio wake wa kwanza.

Mara nyingi huu ndio mwitikio wetu wa kwanza pia.  Tunataka kuwa waaminifu na tunataka kumfuata Kristo bila kujali anachotuomba.  Lakini tunapopewa mwaliko mahususi wa kuitikia wito Wake, tunageuka na kuondoka kwa huzuni, tukifikiri kwamba mwaliko huo unatudai mengi mno.

Tafakari leo kuhusu huyu kijana tajiri.  Tazama maisha yako mwenyewe na ujiulize ni kwa kiasi gani uko tayari na una nia ya kusema “Ndiyo” kikamilifu kwa chochote Yesu anachokuomba.  Kusema “Ndiyo” kwa kujitoa sadaka ndiyo uamuzi bora zaidi unaoweza kufanya.  Kwa hakika, ni kuyakubali kwa hiari maisha yenye utukufu mkuu zaidi unayoweza kuishi.

Bwana wangu unayenidai mengi, kukufuata Wewe wakati mwingine kunaweza kuonekana kuwa kugumu na kuhitaji kujitoa bila kujibakiza.  Kunaweza kuonekana kana kwamba kunanidai mengi mno.  Unisaidie, hasa katika nyakati hizo, nikutumainie Wewe kuliko mambo mengi niliyoshikamana nayo katika ulimwengu huu.  Yesu, nakutumainia.

Sala za Kuomba Amani

Komesha Vita…Nyumbani—Video
Bibi Yetu wa Fatima anatuita tusali rozari kwa ajili ya amani

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Mwaka

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha iliyoangaziwa hapo juu: Heinrich Hofmann, “Kristo na Mtawala Kijana Tajiri”, kupitia Wikimedia Commons


Vitabu viwili bora kwa Kwaresima:

Tafakari za Kwaresima na Pasaka
Zimesasishwa kwa ajili ya Kwaresima & Pasaka 2022 kwa kuongezwa tafakari nyingine na Orodha ya Yaliyomo yenye maelezo ya kina zaidi

Tafakari za Kwaresima na Pasaka ni kimoja kati ya vitabu vinne vinavyounda Mfululizo wa Tafakari za Kila Siku za Kikatoliki. Kikiwa kitabu cha kukuza maisha ya kiroho, ni nyenzo bora kwa tafakari na sala za kila siku, kikitoa tafakari kuhusu Injili ya siku kwa namna inayohusiana na maisha ya vitendo, iliyo aminifu kwa imani na inayoeleweka kwa urahisi. Kimepangwa kwa namna inayowezesha kutumiwa katika mwaka wowote wa kiliturujia, kikitoa tafakari kwa kila chaguo la Injili, yakiwemo yale ya Jumapili katika Miaka A, B & C, kila chaguo la Misa Takatifu ya kila siku, na Sikukuu na Sherehe zote. Ruhusu kifo na ufufuko wa Kristo viubadilishe moyo wako kwa ukamilifu zaidi katika Kwaresima na Pasaka hii!  Kinapatikana pia katika mfumo wa kitabu chenye jalada laini & kitabu cha kielektroniki!

Siku 40 Chini ya Msalaba:
Mtazamo wa Upendo kutoka Moyoni mwa Mama Yetu Mwenye Heri

Kupitia kitabu hiki cha ibada ya kila siku, unaalikwa kutafakari kwa sala mawazo na moyo wa Mama yetu Mwenye Heri alipovumilia mateso makali aliyotendewa Mwanawe mwenyewe mpendwa.  Mama Maria aliukabili Msalaba wa Mwanawe kwa imani, upendo na moyo wa kujitoa ulio kamili. Uaminifu wake kwa Mwanawe katika maisha Yake yote haukuyumba. Aliposimama mbele ya Msalaba katika muda ule mrefu wa saa tatu, uaminifu huo haukukoma kamwe.