Kiswahili

Watendee Wengine…

21 Juni 2022
Jumanne ya Wiki ya Kumi na Mbili ya Kipindi cha Kawaida
Masomo ya Leo

Mtakatifu Aloisi Gonzaga, Mtawa—Kumbukumbu

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

“Watendeeni wengine yote mnayotaka wao wawatendee ninyi. Hii ndiyo Sheria na Manabii.”  Mathayo 7:12

Maneno haya tunayoyafahamu sana yalikuwa amri kutoka kwa Mungu iliyowekwa katika Agano la Kale.  Ni kanuni nzuri ya kuongoza maisha.

Ungependa wengine “wakutendee” nini?  Tafakari jambo hilo na ujaribu kuwa mkweli.  Tukiwa wakweli, lazima tukiri kwamba tunataka wengine watufanyie mengi.  Tunataka kuheshimiwa, kutendewa kwa hadhi, kutendewa kwa haki, na kadhalika.  Lakini katika undani zaidi wa mioyo yetu, tunataka kupendwa, kueleweka, kujulikana na kutunzwa.

Ndani ya mioyo yetu, sote tunapaswa kujitahidi kutambua shauku ya kiasili ambayo Mungu ametupa ya kuwa na uhusiano wa upendo na wengine, na ya kupendwa na Mungu.  Shauku hii inagusa kiini cha maana ya kuwa binadamu.  Sisi binadamu tumeumbwa kwa ajili ya upendo huo.  Kifungu hiki cha Maandiko Matakatifu kilicho hapo juu kinafunua kwamba tunapaswa kuwa tayari na kuwa na nia ya kuwapa wengine kile tunachotamani kupokea.  Ikiwa tunaweza kutambua ndani yetu shauku ya kiasili ya kupendwa, tunapaswa pia kujitahidi kukuza shauku ya kupenda.  Tunapaswa kukuza shauku ya kupenda kwa kiwango kilekile tunachotamani sisi wenyewe kupendwa.

Hili ni gumu zaidi kuliko linavyoonekana.  Mwelekeo wetu wa ubinafsi ni kudai na kutarajia upendo na huruma kutoka kwa wengine, huku sisi wenyewe tukijiridhisha na kutoa kidogo zaidi.  Jambo la msingi ni kuelekeza fikira zetu kwanza kwenye wajibu wetu.  Tunapaswa kujitahidi kutambua kile tunachoitwa kufanya na namna tunavyoitwa kupenda.  Tunapoliona hili kuwa wajibu wetu wa kwanza na kujitahidi kuliishi, tutagundua kwamba tunapata uradhi mkubwa zaidi katika kutoa kuliko katika kutafuta kupokea.  Tutatambua kwamba “kuwatendea wengine,” bila kujali yale “wanayotutendea,” ndiko kunakotupa utimilifu wa kweli.

Tafakari leo juu ya shauku ya kiasili iliyo moyoni mwako ya kupendwa na kuheshimiwa na wengine.  Kisha, ifanye shauku hii kuwa mwongozo wa namna unavyowatendea walio karibu nawe.

Bwana wa matamanio makamilifu, nisaidie niwatendee wengine yale ninayotamani wanitendee mimi.  Nisaidie nitumie hamu ya upendo iliyo moyoni mwangu kama msukumo wa kuwapenda wengine.  Ninapojitoa, nisaidie nipate utimilifu na kuridhika katika kujitoa huko.  Yesu, nakutumainia.

Uamsho wa Kitaifa wa Ekaristi
Unaanza 19 Juni 2022—Sherehe ya Mwili na Damu ya Kristo

Novena kwa Moyo Mtakatifu wa Yesu
Tarehe za Novena: Juni 15-23, 2022
Juni 24, 2022: Sherehe ya Moyo Mtakatifu wa Yesu

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu Zote

Mtakatifu wa Siku – Mtakatifu Aloisi Gonzaga, Mtawa

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha iliyoangaziwa hapo juu: Kugeuka Sura, Duccio di Buoninsegna, kupitia Wikimedia Commons