Kiswahili

Kuyakimbilia Mapenzi ya Mungu

Jumatano, Desemba 20, 2023
Siku ya Juma ya Majilio
Masomo ya Leo

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

Naye malaika akamjibu, “Roho Mtakatifu atakujilia, na nguvu za Aliye Juu zitakufunika kwa uvuli wake. Kwa hiyo mtoto atakayezaliwa ataitwa mtakatifu, Mwana wa Mungu.” Luka 1:35

Jaribu kuweka kando yote unayoyajua kumhusu Yesu na kutafakari tu maneno haya ya Malaika Mkuu Gabrieli kana kwamba unayasikia kwa mara ya kwanza kama alivyoyasikia Mama yetu Mwenye Heri. Aliambiwa kwamba angepata mtoto, ingawa hakuwa amekutana kimwili na mwanamume. Aliambiwa kwamba mimba hii ingetungwa kwa kufunikwa na uvuli wa Roho Mtakatifu. Naye aliambiwa kwamba Mtoto wake angekuwa Mwana wa Mungu. Maria angeyaelewaje mafunuo haya ya ajabu aliyopewa na Malaika huyu Mkuu mwenye utukufu mwingi sana?

Mtu wa kawaida huenda angehitimisha kwamba haya yalikuwa aina fulani ya maono ya udanganyifu na kwamba yale aliyokuwa akiyaona na kuyasikia yalitokana na tatizo fulani la kisaikolojia la muda mfupi. Labda Maria alikuwa akiota ndoto? Au labda kulikuwa na kitu alichokula au kunywa bila kujua ambacho kilimfanya apitie hali hii?

Lakini Mama yetu Mwenye Heri hakuwa mtu wa kawaida, wala akili yake haikuwa ya kawaida. Akili yake ilikuwa angavu kikamilifu kwa sababu ya asili yake isiyo na doa la dhambi. Na akili yake daima ilikuwa “imejaa neema,” kama Gabrieli alivyosema alipomsalimu. Aliijua sauti ya Mungu, na alijua kwamba Malaika huyu Mkuu alikuwa akimpa ujumbe kutoka juu. Kwa hiyo, alisikiliza, akapokea, akaamini na kukubali.

Tunaweza pia kuhitimisha kwamba Maria alifanya hata zaidi ya kukubali tu. Upendo aliokuwa nao kwa Mungu na kwa mapenzi Yake ungekuwa mkubwa sana kiasi kwamba angejawa mara moja na shauku inayowaka ya kutimiza agizo hili la Malaika Mkuu. Angejawa na shauku takatifu ya kufanya yote aliyoweza ili kutimiza wito huu wa kimiujiza aliokuwa ameupokea. Na wito huu ungekuwa mara moja kusudi kuu la maisha yake.

Ingawa hakuna hata mmoja wetu aliyepewa wito wa pekee na wenye utukufu aliopewa Mama yetu Mwenye Heri, hakika sisi sote tumepewa utume na Mungu. Wakati mwingine tunasikiliza na kuutafakari. Wakati mwingine tunachagua kuukubali kwa moyo wote. Lakini lililo bora ni kumwiga Mama yetu Mwenye Heri na kuukimbilia. Haitoshi tu kuwa tayari kuupokea. Haitoshi tu kujisalimisha. Lazima pia turuhusu kila tamanio ndani ya roho zetu, kila shauku tuliyo nayo na kila hamu ndani yetu vielekee katika kutimiza mapenzi ya Mungu.

Ni nini Mungu anakuita ufanye maishani? Kusudi lako ni lipi? Utume wako ni upi? Ikiwa unaona ugumu kujibu maswali haya, basi labda anza kwa kuomba upewe shauku takatifu ya kina inayokuteka kabisa, ili kutimiza kile ambacho Mungu amekuchagulia. Ikiwa jambo pekee unalotamani ni kutimizwa kwa mapenzi ya Mungu, basi Mungu atakapokufunulia mapenzi Yake, utaweza kuyatimiza kwa urahisi zaidi na kwa haraka zaidi.

Tafakari leo juu ya utume wa pekee ambao Mungu amekupa. Chochote alichokuita ufanye katika maisha yako ni wito uliopewa wewe tu. Usiukimbie. Usiukubali kwa shingo upande. Badala yake, ukimbilie kwa nafsi yako yote na umruhusu Mungu afanye mambo makuu kupitia wewe.

Bwana mtakatifu kabisa, najua kwamba una mpango mkamilifu kwa ajili ya maisha yangu. Najua kwamba umenipa utume ambao hajapewa mtu mwingine yeyote. Tafadhali ijaze roho yangu kwa wingi wa shauku takatifu ya kuyatimiza kikamilifu mapenzi Yako, na kufanya hivyo kwa kujitolea kwa bidii kubwa kabisa na kwa nguvu zote. Mimi pia ni mtumishi Wako, Ee Bwana; na iwe kwangu kadiri ya mapenzi Yako. Mama Maria, utuombee.  Yesu, nakutumainia.

Mpya kwa 2024!
Zawadi nzuri sana ya Krismasi…

Novena ya Krismasi ya Mtakatifu Andrea
Kwa desturi husaliwa mara 15 kwa siku kuanzia Novemba 30 hadi mkesha wa Krismasi.

Antifona za “Ee” za Majilio
Desemba 17–23

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Majilio

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha iliyoangaziwa hapo juu:Kupashwa Habari, kazi ya Philippe de Champaigne, kupitia Wikimedia Commons