Kiswahili

Chachu Yako Ni Ipi?

15 Februari 2022
Jumanne ya Juma la Sita la Mwaka
Masomo ya Leo

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

Yesu aliwaonya, “Angalieni, jilindeni na chachu ya Mafarisayo na chachu ya Herode.”  Marko 8:15

Ni nini hii “chachu” ambayo Yesu anaizungumzia?  Baada ya kuwapa wanafunzi Wake onyo hili, Yesu anawaeleza anachomaanisha na asichomaanisha.  Lakini hata maelezo hayo yanaonekana kuwashinda kuelewa.  Kwa hiyo anamalizia kwa kusema, “Je, bado hamwelewi?”  Hadi leo, Yesu bado anamuuliza kila mmoja wetu swali hili.

Bila shaka, hapa Yesu alikuwa akijaribu kuwafanya wafikiri, wasikilize na watazame kwa undani zaidi.  Alikuwa akiwaonya, “Angalieni!”  Jihadharini na chachu hii.  Ni onyo la upendo la kuwasaidia kuona na kuelewa hatari iliyo halisi kabisa.

Kila anayeoka mkate anajua athari ya chachu kidogo tu (kama vile hamira) katika donge la unga.  Ukiweka kiasi kidogo tu, kinaathiri mkate mzima.  Mtoto akiwa anasaidia kuoka, anaweza kurudi mara kadhaa kutazama jinsi donge linavyofumuka kidogo kidogo.  Kutazama jambo hilo kunaweza kuvutia sana.  Na yote hayo yametokana na hamira hii kidogo tu.

Basi, chachu hii ya Mafarisayo na Herode ni nini?  Ni maneno maovu, nia mbaya na upotovu wanaoeneza.  Kwa Mafarisayo, huenda ni kuelewa vibaya kidogo tu au kupotosha kidogo yale ambayo Yesu alisema au alifanya.  Wanaweza kupindisha maneno Yake au kuwapa wengine maoni yao bila hata kusema neno.  Hali hii huambukiza na inaweza kuathiri kila mtu.  Kidogo kidogo, mbegu zao ndogo za mashaka na upinzani huwaletea wengine madhara.

Huenda tukawa na mwelekeo wa kuwafikiria watu wote “wale” tunaowajua wanaofanya hivi.  Lakini tungekosa nafasi muhimu ya kukua ikiwa tungeshindwa kujitazama wenyewe kwanza.  Je, mimi hufanya hivi wakati mwingine?  Je, ninasema mambo yanayopotosha kwa namna ndogo au zisizo rahisi kutambua?  Au ninawapotosha wengine kwa mitazamo yangu hasi ninayoionyesha bila maneno?  Je, wakati mwingine mimi ni “mtu mwenye mtazamo hasi”?

Hakuna haja ya kujihisi wenye hatia au kujivunja moyo tunapotambua kwamba tumekosea.  Badala yake, tunapaswa kulitafakari fundisho hili dogo la Yesu ili tutambue nguvu kubwa ya maneno yetu.  Hata maneno machache kabisa yanaweza kuleta madhara makubwa kadiri muda unavyopita.

Lakini si hilo tu tunalopaswa kuzingatia.  Ni muhimu vilevile kutambua kwamba maneno machache ya upendo tunayosema pia yanaweza kuleta mabadiliko makubwa kadiri muda unavyopita.  Labda ni tabasamu lile dogo tu tunalotoa au tendo la wema ambalo tunadhani halionekani na mtu.  Matendo na maneno haya madogo ndiyo chachu ya Injili.  Kwa kweli huleta mabadiliko, na yanaweza pia kuenea kutoka kwa mtu mmoja hadi kwa mwingine.

Tafakari leo mambo madogo ya maisha.  Jua kwamba dhambi hizi ndogo na matendo madogo ya upendo huleta tofauti kubwa hatimaye.

Bwana wangu mwenye kunitilia maanani, nisaidie kuwa mwaminifu na kuona ni chachu ya aina gani ninayopanda kila siku.  Nisaidie kutakaswa na ubaya na kujazwa wema.  Univuvie kuwa chachu hiyo njema katika mawasiliano yangu yote mengi ya kila siku.  Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Mwaka

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha kuu hapo juu: Yesu Akihubiri Ndani ya Meli, iliyochorwa na James Tissot, kupitia Makumbusho ya Brooklyn