Kiswahili

Wasiwasi wa Dhamiri Uliopitiliza

3 Septemba 2022
Jumamosi ya Juma la Ishirini na Mbili la Mwaka
Masomo ya Leo

Mtakatifu Gregori Mkuu, Papa na Mwalimu wa Kanisa—Kumbukumbu

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

Yesu alipokuwa akipita katika shamba la nafaka siku ya Sabato, wanafunzi wake walikuwa wakichuma masuke, wakiyapukusa mikononi mwao na kula nafaka zake. Baadhi ya Mafarisayo wakasema, “Kwa nini mnafanya jambo lisiloruhusiwa siku ya Sabato?” Luka 6:1-2

Huku ndiko kushikilia mambo madogo yasiyo na maana! Hapa wanafunzi walikuwa na njaa; yaelekea walikuwa wametembea kwa muda pamoja na Yesu, wakakuta ngano na kuchuma ili wale walipokuwa wakitembea. Nao wakalaumiwa na Mafarisayo kwa kufanya jambo hili la kawaida kabisa. Je, kweli walivunja sheria na kumkosea Mungu kwa kuchuma na kula nafaka hizi?

Jibu la Yesu linaweka wazi kwamba Mafarisayo wamechanganyikiwa sana na kwamba wanafunzi hawakufanya kosa lolote. Lakini kifungu hiki kinatupa nafasi ya kutafakari juu ya hatari moja ya kiroho ambayo wengine huangukia nyakati fulani. Ni hatari ya wasiwasi wa dhamiri uliopitiliza.

Hatujui kama ndivyo ilivyokuwa, lakini ikiwa mwanafunzi mmoja au zaidi walikuwa wakipambana na wasiwasi wa dhamiri uliopitiliza, kisha wakawasikia Mafarisayo wakiwalaumu kwa kula nafaka, huenda walijuta mara moja na kujihisi kuwa na hatia kwa matendo yao. Wangeanza kuogopa kwamba walikuwa na hatia ya kuvunja amri ya Mungu ya kuitakasa Sabato. Lakini wasiwasi wao wa dhamiri uliopitiliza unapaswa kuonekana jinsi ulivyo, nao wanapaswa kutambua kichocheo kilichowashawishi kuingia katika wasiwasi huo.

“Kichocheo” kilichowatia kishawishini ni mtazamo uliopitiliza na wenye makosa kuhusu sheria ya Mungu kama ilivyowasilishwa na Mafarisayo.  Naam, sheria ya Mungu ni kamilifu na lazima ifuatwe daima hadi herufi yake ya mwisho.  Lakini kwa wale wanaosumbuliwa na wasiwasi uliopitiliza wa dhamiri, sheria ya Mungu inaweza kupotoshwa na kukuzwa kupita kiasi kwa urahisi.  Sheria za kibinadamu na maelezo ya kibinadamu yanayopotosha sheria ya Mungu yanaweza kusababisha mkanganyiko.  Na katika kifungu cha Maandiko hapo juu, kichocheo kilikuwa kiburi na ukali wa Mafarisayo.  Mungu hakuchukizwa kwa namna yoyote na wanafunzi kuchuma na kula nafaka siku ya Sabato.  Kwa hiyo, Mafarisayo walikuwa wakijaribu kuwatwika wanafunzi mzigo ambao haukutoka kwa Mungu.

Sisi pia tunaweza kushawishika kuitazama sheria ya Mungu na mapenzi yake kwa wasiwasi wa dhamiri uliopitiliza. Ingawa watu wengi hufanya kinyume chake, yaani, hulegeza mambo kupita kiasi, wengine hupambana na hofu ya kumkosea Mungu wakati ambapo hawamkosei hata kidogo.

Tafakari leo juu ya pambano lako mwenyewe dhidi ya wasiwasi wa dhamiri uliopitiliza. Ikiwa hii ndiyo hali yako, ujue kwamba Mungu anataka kukuweka huru kutoka katika mizigo hii.

Bwana, nisaidie kuona sheria Yako na mapenzi Yako katika mwanga wa ukweli.  Nisaidie kuachana na dhana zote potofu na maelezo yote yanayopotosha sheria Yako, na badala yake nikubali kweli za upendo na huruma Yako kamilifu.  Na nishikamane na huruma na upendo huo katika mambo yote na kuliko mambo yote.  Yesu, nakutumainia.

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu Zote

Mtakatifu wa Leo – Mtakatifu Gregori Mkuu, Papa na Mwalimu wa Kanisa

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha: Mandhari pana ya Biblia, au Maandiko Matakatifu katika picha na masimulizi, kupitia Wikimedia Commons