Desemba 17, 2023
Jumapili ya Tatu ya Majilio (Mwaka B)
Masomo ya Leo

Sikiliza kwa Kiingereza
“Mimi ni sauti ya mtu anayepaza sauti jangwani, ‘nyosheni njia ya Bwana,’” kama alivyosema nabii Isaya.” Yohane 1:23
Katika kifungu hicho hapo juu, Mtakatifu Yohane Mbatizaji ananukuu Isaya 40:3: “Sauti inatangaza: Jangwani itayarisheni njia ya BWANA! Nyosheni nyikani barabara kuu kwa ajili ya Mungu wetu!” Huu ulikuwa unabii wa Isaya, aliyekuwa akizungumzia kurudi kwa Wayahudi waliokuwa uhamishoni Babeli kwenda Yerusalemu. Kwa kawaida, watu wangesafiri kwa kufuata njia zenye maji ya kutosha kutoka Mesopotamia kwenda Israeli. Njia hizo zilikuwa salama zaidi kuliko jangwa na ziliwapatia chakula na maji waliyohitaji kwa safari. Lakini Isaya alitabiri kwamba Wayahudi waliokuwa uhamishoni wangesafiri kwa njia fupi zaidi—moja kwa moja kupitia jangwani—na kwamba Mungu angewapatia mahitaji yao katika safari hiyo. Safari ya namna hiyo ilihitaji kutumainia sana maongozi ya Mungu.
Yohane Mbatizaji, anapomnukuu Isaya, anauhusisha unabii huu na yeye mwenyewe. Aliitwa kupaza sauti jangwani na kuwaelekeza watu moja kwa moja kwa Masiya. Ni jangwani ambapo wangempata Mwokozi wao.
Kwanza kabisa, Yohane anapaza sauti “jangwani.” Ujumbe wake ni kwa wale wanaopitia hali ya ukavu, ufukara, uhitaji na kupoteza vitu maishani kwa sababu ya dhambi. Ujumbe wake wa toba unawalenga kwanza wale wasio na lishe ya kiroho ambayo Mungu anataka kuwajalia kwa njia ya neema. Ujumbe wa Yohane unaelekezwa kwa wale wanaotambua kwa unyenyekevu hali ngumu wanayokabiliana nayo maishani na kukiri hitaji lao la Maji yaliyo Hai ya Mwokozi wa Ulimwengu.
Pili, njia hii mpya “iliyonyooka” inadokeza kwamba wengi hawatembei katika njia inayowaongoza moja kwa moja kwa Kristo. Badala yake, wanapita katika njia za mzunguko zisizo za lazima maishani. Ujumbe wa Yohane unamwita kila mtu kwenye njia iliyonyooka na ya moja kwa moja ya kutubu dhambi zake ili aweze kumwamini Kristo Yesu.
Tatu, kutembea kupitia jangwani ili kumpata Kristo kunahitaji kutumainia maongozi ya Mungu. Inahitaji ujasiri kufanya safari ya namna hiyo. Jambo la msingi ni kutumainia maongozi ya Mungu yasiyokoma, Yeye anayeahidi kutupatia mahitaji yetu yote. Mtu asingepita moja kwa moja jangwani ikiwa hakumtumaini kiongozi wake.
Majilio ni wakati wa kuichunguza upya njia unayoiendea. Je, unajaribu kutafuta njia yako mwenyewe ya kupata furaha? Je, unategemea uwezo wako mwenyewe, akili yako mwenyewe na mpango wako mwenyewe wa siku zijazo? Ikiwa ndivyo, basi sikiliza “sauti ya mtu anayepaza sauti jangwani.” Msikilize Mtakatifu Yohane akizungumza nawe, akikuita kwenye maisha sahili ya jangwani, kwenye kutofungamana zaidi na vitu vyote, kwenye kuacha yote yasiyotoka kwa Mungu, na kwenye utayari mkubwa zaidi wa kutumainia maongozi ya Mungu yakuongoze.
Tafakari leo juu ya mwito huu kutoka jangwani na usikilize ujumbe ambao Mungu anakuambia wewe binafsi. Acha mahangaiko yote ya kidunia, tubu dhambi, mtumainie Yeye na utoke kwenda kukutana Naye ili uweze kuifikia imani ya kina zaidi katika Bwana wetu kwa haraka na urahisi zaidi katika kipindi hiki cha Majilio.
Bwana wangu mwenye upendo, Wewe upo hapo, ukiningoja katika giza na ukavu wa dhambi yangu. Unaningoja ili uniongoze na kunielekeza katika changamoto nyingi ninazokabiliana nazo maishani. Tafadhali nijalie ujasiri na hekima ninazohitaji ili nikutumainie kiasi cha kukufuata popote unaponiongoza. Yesu, nakutumainia.
Mpya kwa 2024!
Zawadi nzuri sana ya Krismasi…
Antifona za “Ee” za Majilio
Desemba 17–23
Novena ya Krismasi ya Mtakatifu Andrea
Kwa mapokeo, husaliwa mara 15 kwa siku kuanzia 30 Novemba hadi Mkesha wa Krismasi.
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Tazama nyenzo zetu za Majilio!
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu




