Kiswahili

Unyenyekevu + Imani = Huruma

Agosti 3, 2022
Jumatano ya Juma la Kumi na Nane la Kipindi cha Mwaka
Masomo ya Leo

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

Lakini yule mwanamke alikuja akamsujudia, akisema, “Bwana, nisaidie.” Naye akajibu, “Si vema kuchukua chakula cha watoto na kuwatupia mbwa.” Mwanamke akasema, “Tafadhali, Bwana, maana hata mbwa hula makombo yanayoanguka kutoka mezani pa mabwana wao.”  Mathayo 15:25-27

Je, kweli Yesu alimaanisha kwamba kumsaidia mwanamke huyu kulikuwa kama kuwatupia mbwa chakula?  Wengi wetu tungeudhika sana kwa maneno ya Yesu kwa sababu ya kiburi chetu.  Lakini aliyosema yalikuwa kweli, wala hayakuwa ya kifidhuli kwa namna yoyote.  Ni wazi kwamba Yesu hawezi kuwa mfidhuli.  Hata hivyo, kwa juu juu, kauli Yake inaonekana kuwa ya kifidhuli.

Kwanza, tuangalie jinsi kauli Yake ilivyo ya kweli.  Mwanamke huyu alikuwa akimwomba Yesu aje kumponya binti yake.  Kimsingi, Yesu anamwambia kwamba hastahili neema hii kwa namna yoyote.  Na huo ndio ukweli.  Kama vile mbwa asivyostahili kulishwa kutoka mezani, sisi pia hatustahili neema ya Mungu.  Ingawa hii ni namna ya kushtua ya kueleza jambo hilo, Yesu anasema hivyo ili kwanza kuonyesha ukweli wa hali yetu ya dhambi na kutostahili kwetu.  Na mwanamke huyu anakubali hilo.

Pili, kauli ya Yesu inampa mwanamke huyu nafasi ya kuitikia kwa unyenyekevu na imani kubwa kabisa.  Unyenyekevu wake unaonekana katika kutokataa kwake kufananishwa na mbwa anayekula kutoka mezani.  Badala yake, anaeleza kwa unyenyekevu kwamba hata mbwa hula makombo.  Ama kweli, huu ni unyenyekevu!  Kwa hakika, tunaweza kuwa na uhakika kwamba Yesu alizungumza naye kwa namna hii iliyomshusha kiasi kwa sababu alijua jinsi alivyokuwa mnyenyekevu, na alijua kwamba angeitikia kwa kuuacha unyenyekevu wake uangaze ili kuidhihirisha imani yake.  Hakuudhishwa na ukweli uliomnyenyekeza kuhusu kutostahili kwake; badala yake, aliukubali na pia akatafuta huruma tele ya Mungu licha ya kutostahili kwake.

Unyenyekevu una uwezo wa kuifungua njia kwa imani, nayo imani huifungua njia kwa huruma na nguvu za Mungu kutenda kazi.  Mwishowe, Yesu anasema ili wote wasikie, “Ee mwanamke, imani yako ni kubwa!”  Imani yake ilidhihirika, naye Yesu akaitumia nafasi hiyo kumheshimu kwa sababu ya imani hiyo yenye unyenyekevu.

Tafakari leo kuhusu unyenyekevu wako mwenyewe mbele za Mungu.  Ungeitikiaje kama Yesu angezungumza nawe kwa namna hii?  Je, ungekuwa na unyenyekevu wa kutosha kukiri kutostahili kwako?  Ikiwa ndivyo, je, ungekuwa pia na imani ya kutosha kuililia huruma ya Mungu licha ya kutostahili kwako?  Sifa hizi nzuri sana huenda pamoja (unyenyekevu na imani) na kuifungua njia kwa huruma ya Mungu kutenda kazi!

Bwana wangu mwenye huruma kuu, sistahili.  Nisaidie kutambua hilo.  Nisaidie kutambua kwamba sistahili neema Yako maishani mwangu.  Lakini katika ukweli huo wa unyenyekevu, na nitambue pia wingi wa huruma Yako, wala nisiogope kamwe kukuomba huruma.  Yesu, nakutumainia.

Kipindi cha Kawaida: Wiki 18-34

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu

Picha iliyoangaziwa hapo juu: Mwanamke Mkanaani Miguuni pa Kristo Imechorwa na Jean Germain Drouais, kupitia Wikimedia Commons