Kiswahili

Shukrani kwa Baraka Zisizopimika – Kuwa Tayari, Daima

Alhamisi, 28 Novemba 2024
Masomo ya Leo

Marekani: Siku ya Shukrani—Kumbukumbu ya Hiari
(Katika nchi nyingine mbali na Marekani, tazama tafakari ya Alhamisi ya Juma la Thelathini na Nne)

James Tissot, Miliki ya umma, kupitia Wikimedia Commons

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

“Je, hawakutakaswa wote kumi? Wale wengine tisa wako wapi? Je, hakuna aliyerudi kumshukuru Mungu isipokuwa huyu mgeni?” Kisha akamwambia, “Simama, uende zako; imani yako imekuokoa.” Luka 17:17–19

Aliokolewa kwa imani kupitia tendo la kuonyesha shukrani! Ni simulizi zuri ajabu la kutafakari leo tunapoadhimisha sikukuu ya kitaifa ya Shukrani!

Ingawa Siku ya Shukrani si sikukuu maalumu ya Kanisa, bila shaka shukrani ni jambo la msingi katika imani yetu ya Kikristo, kama inavyoonyeshwa katika Injili ya leo ambamo Yesu aliwaponya watu kumi wenye ukoma. Na namna walivyoitikia wakiwa kundi ni jambo la kuzingatia. Tisa kati yao waliponywa wakaenda zao kuendelea na shughuli zao, bila kurudi kwa aliyewaponya ili kumshukuru. Lakini mmoja alirudi. Huyu mtu mmoja mwenye ukoma, ambaye ghafla hakuwa tena na ukoma, alimrudia Yesu, akamtukuza, akaanguka miguuni Pake na kumshukuru. Mtu huyu alikuwa mgeni, Msamaria, lakini alionyesha imani ambayo sisi sote tunapaswa kujitahidi kuiiga. Imani ya Msamaria huyu ilionekana wazi kwa kuwa alijua kwamba hakupaswa tu kuwa na shukrani kwa neema ya uponyaji, bali pia alipaswa kuonyesha shukrani hizo.

Tunapoadhimisha Siku ya Shukrani, tunakumbushwa kwamba, kati ya mambo yote tunayopaswa kuyashukuru, hakuna lililo muhimu kuliko shukrani zetu kwa Mungu kwa neema zisizopimika alizotujalia. Lakini kama simulizi hili linavyoonyesha, ni rahisi sana kupuuza umuhimu wa jinsi tunavyoitikia baraka za Mungu. Ni asilimia kumi tu ya wale wenye ukoma walioitikia kwa kuonyesha shukrani namna hiyo. Kwa hiyo, inafaa leo kuchunguza sababu nyingi zinazotupasa kuwa na shukrani na kujitahidi kumwonyesha Mungu shukrani hizo.

Kwanza, Mungu alituumba kwa upendo. Hii si zawadi ndogo. Ni zawadi ya kwanza aliyotupa, ambayo mara nyingi tunaichukulia kama jambo la kawaida tu. Mungu hakuwa na haja ya kutuumba. Hakuwa na haja ya kukuumba wewe. Lakini alikuumba. Na zawadi ya uhai, zawadi ya roho isiyokufa, ni jambo ambalo hatupaswi kamwe kulipuuza, bali tunapaswa kulifurahia daima.

Pili, Mungu aliingia katika hali yetu ya kuanguka dhambini kwa kujifanya mwili katika tumbo la Bikira Maria Mwenye Heri. Kwa kufanya hivyo, aliinua asili yetu ya kibinadamu iliyoanguka dhambini hadi kiwango kisichowahi kujulikana hapo awali. Ubinadamu na umungu viliunganishwa katika Nafsi ya Mwana wa Mungu na Mwana wa Mtu aliyejifanya mwili, nasi tunapaswa kushukuru kwa zawadi hii tusiyostahili, inayotujaza mshangao na kicho.

Tatu, tunajua yaliyofuata katika simulizi hili. Mungu, katika Nafsi ya Mwana aliyejifanya mwili, aliteseka, akafa na akafufuka. Kwa kufanya hivyo, aliwezesha kila dhambi yetu kufutwa. Tunapokufa pamoja Naye, tunaalikwa kufufuka pamoja Naye. Na tunapofufuka pamoja Naye, tunaalikwa kushiriki utukufu Wake Mbinguni.

Mwisho, katika maisha ya kila mmoja wetu, kuna neema zisizohesabika tunazopewa kila siku. Lakini kama watoto waliodekezwa, mara nyingi tunazipuuza baraka hizi na kuzichukulia kama jambo la kawaida tu. Kutoa mifano hapa hakutoshi. Ikiwa unataka kuwa na moyo wenye shukrani, ni muhimu ujifunze kuziona baraka hizi katika maisha yako mwenyewe. Mara nyingi sana tunaelekeza fikira zetu kwenye mapambano na maumivu yetu. Lakini baraka ni nyingi, na kadiri tunavyomgeukia Bwana wetu kwa kujikabidhi Kwake kabisa, ndivyo baraka zinavyozidi kumiminika.

Tafakari leo kuhusu mtazamo ulio nao kwa baraka nyingi ambazo Mungu amekujalia. Anza kwa kuzingatia baraka za msingi za uumbaji wa Mungu na matendo Yake ya upendo yanayoleta wokovu. Kisha jaribu kutafakari njia nyingi ndogondogo ambazo Mungu amekuwa pamoja nawe, amekuongoza, amekuimarisha na kukubariki kwa wingi. Ikiwa huyaoni mambo haya wazi, basi tumia siku hii kusikiliza kwa makini ili Mungu akufunulie hayo. Unapoziona baraka zako, itikia kama huyu mtu mmoja aliyekuwa na ukoma. Mgeukie Yesu, umtukuze, uanguke miguuni Pake katika sala na kumshukuru. Kufanya hivyo kutakujaza imani ileile iokoayo aliyojaliwa mtu huyu aliyekuwa na ukoma.

Bwana wangu mkarimu mno, umenijalia baraka zinazozidi ninavyoweza kufikiria. Natambua kwamba sitaweza kamwe kuelewa kikamilifu jinsi ulivyokuwa mwema kwangu, wala sitaweza kamwe kuonyesha shukrani zangu ipasavyo. Tafadhali, nijalie moyo uliojaa shukrani. Nisaidie kuona utendaji Wako katika maisha yangu na kukuitikia kama huyu mtu mmoja aliyekuwa na ukoma. Yesu, nakutumainia.

Soma Zaidi – Siku ya Shukrani

Sala na Tafakari za Majilio

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Tafakari za Maandiko Matakatifu kwa Kipindi cha Mwaka

Watakatifu/Sikukuu Zote

Katika nchi nyingine mbali na Marekani, tazama tafakari ya Alhamisi ya Juma la Thelathini na Nne

Chaguo za Masomo ya Misa Takatifu


Kuwa Tayari, Daima
28 Novemba 2024
Alhamisi ya Juma la Thelathini na Nne la Mwaka
Masomo ya Leo

© José Luiz Bernardes Ribeiro

Video

Sikiliza kwa Kiingereza

“Ndipo watakapomwona Mwana wa Mtu akija katika wingu kwa nguvu na utukufu mkuu. Lakini ishara hizi zitakapoanza kutokea, simameni wima na kuinua vichwa vyenu, kwa sababu ukombozi wenu umekaribia.”  Luka 21:28

Kifungu hiki hapo juu kinahitimisha mfululizo wa mafundisho ya Yesu kuhusu mateso na dhuluma zitakazotokea katika ulimwengu huu. Lakini mafundisho Yake yanahitimishwa kwa maneno hayo hapo juu, yanayotupa matumaini makubwa tunapotarajia kurudi kwa Yesu katika utukufu. Kifungu hiki kinazungumzia maono ya kinabii ya Danieli (Danieli 7:13–14), yaliyomtia Danieli hofu alipoyaona. Alishuhudia dhuluma kubwa zilizokuwa zinakuja, pamoja na kuangamizwa kwa uovu wote kutakakoambatana na kurudi kwa Mwana wa Mtu.

Unapofikiria ujio wa mwisho wa Kristo pamoja na kifo chako mwenyewe kitakachotokea baadaye, ni nini kinachokujia akilini? Ikiwa malaika angekujulisha kwamba kesho ndiyo ingekuwa siku hiyo, siku ambayo Mwana wa Mtu angerudi katika fahari na utukufu Wake wote ili kuukomesha ulimwengu huu na kuuhukumu, ungeitikiaje? Ungeingiwa na hofu kuu? Furaha tele? Matumaini? Kuchanganyikiwa? Labda ungekuwa na kiasi fulani cha kila mojawapo ya hisia hizi. Kuhusu wakati huu, Yesu alisema kwamba “mataifa yangekuwa katika fadhaa” na kwamba “Watu watakufa kwa hofu wakitazamia mambo yanayoujia ulimwengu.” Basi, unaitikiaje siku hii ya Bwana wetu iliyoahidiwa?

Wale ‘watakaokufa kwa hofu’ ni wazi kwamba ni wale watakaokabili siku hii bila kuwa wamejiandaa hata kidogo. Kukutana na Mwana wa Mtu, Mwana wa Mungu, Mwokozi wa Ulimwengu na Hakimu wa Milele ukiwa hujajiandaa hata kidogo ni jambo la kutisha. Kwa mfano, fikiria kwamba ulikuwa mwenyeji wa karamu kubwa ya chakula cha jioni, lakini ukachanganya siku. Siku yenyewe ikafika, nawe ulikuwa hutarajii mtu yeyote hadi juma lililofuata, lakini wageni wakaanza kuwasili kwa wingi. Fikiria wasiwasi na aibu ambayo ungekuwa nayo. Tukio kama hilo lisingekuwa kitu likilinganishwa na kutokuwa tayari kwa hukumu ya Kristo tutakaposimama mbele Yake wakati wa kifo chetu, na kisha katika Hukumu ya Mwisho mwishoni mwa ulimwengu.

Habari njema ni kwamba, siku hiyo, wale waliojiandaa kweli kwa kuishi maisha ya imani na kutumikia mapenzi ya Mungu bila kujitafutia faida wanaambiwa: “Simameni wima na kuinua vichwa vyenu, kwa sababu ukombozi wenu umekaribia.” Ukifanya yote unayoweza kujiandaa kwa siku hiyo, basi itakuwa siku utakayoitarajia kwa matumaini makubwa sana na shauku. Hakika utaweza kusimama wima, kuelekeza macho yako kwa Hakimu wa Wote anayekuja, na kupokea tuzo ya milele ambayo anatamani sana kukujalia. Lakini utapata hayo tu ikiwa uko tayari kweli kwa siku hiyo kwa kuishi maisha ya kumwiga Kristo kikamilifu.

Tafakari leo juu ya siku hiyo ya mwisho. Fikiria kila mtu aliyewahi kuumbwa akisimama mbele ya Kiti cha Hukumu cha Kristo. Kila dhambi na kila fadhila vitafunuliwa siku hiyo. Mawazo na mioyo ya wote vitaonekana wazi Mungu atakapovifunua kwa wote. Na wale walioishi maisha ya uaminifu watafurahi wanapoona haki ya Mungu na huruma Yake zikiungana hukumu Zake zinapotolewa. Ikiwa siku hii inakutisha, tafakari sababu zake. Ikiwa huitazamii kwa hamu nyakati hii ya uamuzi wa mwisho, basi huenda unahitaji kutafakari kwa undani zaidi mambo unayopaswa kufanya ili kujiandaa kikamilifu. Jiandae leo. Usingoje. Bwana wetu anaweza kurudi wakati wowote. Usije ukakutwa bila kuwa tayari.

Hakimu wangu wa milele, unaahidi kurudi duniani wakati maalumu ili kuleta ukamilifu wa haki. Daima niwe tayari kwa siku hiyo kwa kuishi katika muungano nawe na mapenzi Yako matakatifu. Ninaomba siku hiyo ifike upesi, Bwana mpendwa, na kwamba watoto Wako wote wawe tayari kukutana nawe utakapokuja. Yesu, nakutumainia.

Sala na Tafakari za Majilio

Tafakari Zaidi za Injili

Tafakari juu ya Huruma ya Mungu

Watakatifu/Sikukuu za Leo

Nchini Marekani tazama tafakari ya Siku ya Shukrani

Chaguo za Masomo ya Misa Takatifu