Kiswahili

Sikukuu ya Watoto Watakatifu Wasio na Hatia, Mashahidi

Desemba 28, 2019
Watoto Watakatifu Wasio na Hatia, Mashahidi—Sikukuu
Siku ya Nne ya Oktava ya Krismasi
Masomo ya Leo

Sikiliza kwa Kiingereza

Herode alipotambua kwamba alikuwa amedanganywa na mamajusi, alikasirika sana. Akaamuru wauawe watoto wote wa kiume wenye umri wa miaka miwili na chini ya hapo katika Bethlehemu na maeneo ya jirani, kulingana na wakati aliokuwa ameuthibitisha kutoka kwa mamajusi. Mathayo 2:16

Leo, katika siku ya nne ya Oktava ya Krismasi, tunapewa ushuhuda unaofanana na ule tulioupokea Desemba 26, Sikukuu ya Kifo cha Kishahidi cha Mtakatifu Stefano. Lakini sikukuu ya leo inatuonyesha uovu huohuo kwa namna tofauti na yenye kuhuzunisha hata zaidi. Hapa, kwa kijicho na chuki, Herode aliagiza wauawe watoto wengi wasio na hatia, akijaribu kumwangamiza Yesu, Mfalme aliyezaliwa.

Tunaweza tu kuwazia huzuni ambayo ingelijaa katika mji wa Bethlehemu na maeneo ya jirani huku askari wakipita na kuwaua watoto hao wasio na hatia, wazazi wao wakiangalia bila kuweza kufanya lolote. Kwa upande mmoja, inashtua kujua kwamba Mungu aliruhusu jambo hili. Kwa upande mwingine, kwa imani ya kina, tunapaswa kujitahidi kuelewa ushuhuda walioutoa watoto hawa wasio na hatia.

Ingawa hili lilikuwa tendo la jinai na uovu usioelezeka, kwa mtazamo wa umilele, Mungu atalishughulikia. Mbinguni na hata milele, wahanga hawa wasio na hatia watavaa taji la ushahidi na wataheshimiwa na malaika na watakatifu kama mashahidi wa kwanza wa Mfalme aliyezaliwa. Ingawa huenda jambo hili halikupunguza maumivu wakati ule, hakika litayageuza maumivu ambayo familia hizo zilihisi, watakapoingia katika haki ya Mbinguni.

Ushuhuda wao unatufunulia mengi kuhusu maisha yetu wenyewe. Unatufunulia kwamba kuna nyakati nyingi maishani ambapo mambo hayana usawa wala haki. Mauaji ya watoto hawa wasio na hatia yanatukumbusha kwa nguvu ukweli huu. Lakini jambo moja tunalopaswa kushikilia ni kwamba mwishowe Mungu ataondoa kila dhuluma na kuleta haki. Leo, tunasherehekea sikukuu kwa taadhima kwa heshima ya watoto hawa kama njia ya kusema kwamba Mungu amelugeuza janga hili kuwa jambo lenye utukufu.

Ndivyo ilivyo pia kwa kila mmoja wetu. Hata “janga” lako liwe lipi, ujue kwamba Mwana wa Mungu aliingia katika ulimwengu wetu, akiichukua asili yetu ya kibinadamu iliyoanguka, ili aweze kuyaweka mambo yote sawa.

Tafakari leo juu ya jambo linalokuumiza zaidi katika kipindi hiki cha Krismasi. Hata liwe lipi, leo unaalikwa kuyaunganisha machungu na maumivu yako na huzuni ya familia zilizowapoteza watoto hawa wadogo. Mwache Mungu akutendee yale aliyowatendea wao wote hatimaye. Acha Umwilisho Wake, kifo Chake na Ufufuko Wake viyageuze machungu yako kuwa taji la ushahidi. Mwishowe, Bwana atashinda katika maisha yako ukimruhusu.

Bwana, ninakukabidhi machungu, maumivu na hali yote ya kuchanganyikiwa. Leo ninajiunga na huzuni ya wale waliowapoteza watoto hawa wadogo, nami ninatumaini kwamba maisha yao, wanapotawala sasa Mbinguni pamoja Nawe, ni ishara kwangu ya mambo yajayo. Kuzaliwa Kwako katika ulimwengu wetu kulikuwa ishara kuu kuliko zote kwamba Wewe ni Mwokozi wetu na kwamba unaweza kuyageuza mambo yote kuwa mema. Yesu, ninayakabidhi maisha yangu Kwako, nami ninajua kwamba utaondoa kila dhuluma na kuleta haki. Yesu, nakutumainia.