Novemba 8, 2020
Jumapili ya Thelathini na Mbili ya Kipindi cha Kawaida, Mwaka A
Masomo ya Leo

Sikiliza kwa Kiingereza
“Kwa hiyo, kesheni, kwa maana hamjui siku wala saa.” Mathayo 25:13
Fikiria kama ungejua siku na saa ambayo ungeondoka katika maisha haya. Bila shaka, baadhi ya watu wanajua kwamba kifo kinakaribia, iwe kwa sababu ya ugonjwa au umri. Lakini fikiria jambo hili katika maisha yako mwenyewe. Ingekuwaje kama Yesu angekuambia kwamba kesho ndiyo siku hiyo? Je, uko tayari?
Huenda mambo mengi ya kawaida ya maisha ambayo ungependa kuyashughulikia yangekujia akilini. Wengi wangewafikiria wapendwa wao wote na jinsi jambo hili lingewaathiri. Yaweke hayo yote kando kwa sasa na ulitafakari swali hili kwa mtazamo mmoja tu. Je, uko tayari kukutana na Yesu?
Ukishaondoka katika maisha haya, ni jambo moja tu litakalokuwa na umuhimu. Yesu atakuambia nini? Muda mfupi kabla ya maneno ya Maandiko Matakatifu yaliyonukuliwa hapo juu, Yesu anasimulia Mfano wa Wanawali Kumi. Baadhi yao walikuwa wenye busara na walikuwa na mafuta kwa ajili ya taa zao. Bwana arusi alipofika usiku wa manane, walikuwa tayari kumpokea wakiwa na taa zilizowashwa, naye akawakaribisha. Wale wapumbavu hawakuwa wamejiandaa wala hawakuwa na mafuta kwa ajili ya taa zao. Bwana arusi alipofika, hawakuwepo kumpokea, nao wakasikia maneno haya: “Amina, nawaambia, siwajui ninyi” (Mathayo 25:12).
Mafuta katika taa zao, au kutokuwepo kwake, ni ishara ya mapendo. Ikiwa tunataka kuwa tayari kukutana na Bwana wakati wowote, siku yoyote, ni lazima tuwe na mapendo katika maisha yetu. Mapendo ni zaidi sana ya msisimko au hisia za upendo. Mapendo ni kujitoa kwa dhati kabisa kuwapenda wengine kwa moyo wa Kristo. Ni mazoea ya kila siku tunayoyajenga kwa kuchagua kuwatanguliza wengine, tukiwapa yote ambayo Yesu anatuomba tuwape. Huenda ikawa sadaka ndogo au tendo la kishujaa la kusamehe. Lakini vyovyote iwavyo, tunahitaji mapendo ili tuwe tayari kukutana na Bwana wetu.
Tafakari leo kuhusu watu katika maisha yako ambao Mungu anataka uwapende. Unafanya hivi kwa kiwango gani? Unajitoa kikamilifu kwa kiasi gani? Uko tayari kufika wapi katika kujitoa huko? Chochote kinachokujia akilini kuhusu upungufu wako katika kipawa hiki, kizingatie na umsihi Bwana akupe neema Yake ili wewe pia uwe mwenye busara na tayari kukutana na Bwana wakati wowote.
Bwana, ninaomba kipawa cha mapendo kinachopita uwezo wa asili katika maisha yangu. Tafadhali nijaze upendo kwa wengine na unisaidie kuwa mkarimu sana katika upendo huu. Nisibakize chochote, na kwa kufanya hivyo, niwe tayari kikamilifu kukutana Nawe wakati wowote utakaponita niende nyumbani Kwako. Yesu, nakutumainia.
Tafakari juu ya Huruma ya Mungu
Machaguo ya Masomo ya Misa Takatifu
Picha iliyoangaziwa hapo juu: Mfano wa Wanawali Kumi (sehemu) na Phoebe Anna Traquair




